Dar es Salaam. Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema imemkamata mtuhumiwa wa biashara ya mihadarati, Ayoub Kiboko jijini hapa.
Kiboko ambaye ni mfanyabiashara maarufu ndani na nje ya nchi anadaiwa kumiliki hoteli kubwa zaidi ya 10 pamoja nyumba za kifahari katika maeneo mbalimbali hapa jijini.
Mtuhumiwa huyo ambaye DCEA imesema ilikuwa ikimsaka kwa muda mrefu, alikamatwa pamoja na mkewe Pilli Kiboko Mei 23 saa 8 usiku wakiwa nyumbani kwao eneo la Tegeta.
Kiboko ni miongoni mwa wafanyabiashara waliotajwa katika barua za Watanzania waliofungwa Hong Kong.
Barua hizo zililetwa nchini Desemba 2014 na Kasisi John Wotherspoon anayesaidia wafungwa katika magereza ya Hong Kong na China.
Watanzania hao waliandika barua hizo wakiwaasa wengine wasifanye biashara hiyo huku wakiwataja wafanyabiashara waliowabebesha dawa hizo za kulevya akiwamo Kiboko.
Kamishna wa Operesheni DCEA, Frederick Milanzi alisema jana kwamba walimkamata Kiboko akiwa na dawa za kulevya aina ya heroin, gramu 250 katika msako uliofanywa nyumbani kwake usiku wa manane.
“Baada ya kumkamata mtuhumiwa akiwa na dawa hizo tulitumia vifaa vyetu kupima dawa hizo na tuligungua ni heroin. Lakini anayestahili kutoa majibu ni mkemia mkuu wa Serikali hivyo tumeshapeleka sampuli kwa ajili ya uthibitisho tunasubiri ili ikithibitika mtuhumiwa afikishwe mahakamani,” alisema Milanzi.
Akisimulia namna walivyomkamata Kiboko, Milanzi alisema walipofika katika jumba la kifahari la ghorofa mbili la mtuhumiwa huyo huko Tegeta, waliomba kumkagua lakini alikataa.
“Hata hivyo, maofisa wetu walitumia mbinu zao na kufanikiwa kumkagua kisha kubaini dawa hizo,” alisema.
Alisema katika upekuzi huo walimkuta Kiboko akiwa na bastola ya kichina.
“Lakini tulipoikagua tulibaini anaimiliki bastola hiyo kihalali. Tulimkuta na unga mwingine ambao hatuwezi kutaja ni kiasi gani au ni wa aina gani mpaka utakapopimwa na mkemia mkuu wa Serikali,” alisema
Katika ukaguzi huo, Milanzi alisema walikamata baadhi ya mali za Kiboko yakiwamo magari yake matatu.
Milanzi alidai kuwa mtuhumiwa huyo alianza biashara hiyo muda mrefu na taarifa zinaonyesha kwamba huwatumia vijana mbalimbali kupeleka China.
“Baadhi ya vijana waliohukumiwa kunyongwa China, walimtaja yeye (Kiboko) kuwa ndiye huwatuma,” alisema.
Wakati huo huo; Mkazi wa Mbezi kwa Msuguri, Abdul Omari Salehe (38) alikamatwa Mei 23 katika eneo la kusafiria abiria Bandari ya Dar es Salaam akiwa na pipi 10 za dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 150 alizokuwa akizisafirisha kwenda Zanzibar.
Milanzi alisema mtuhumiwa huyo aliachiwa huru hivi karibuni akitokea gerezani Hong Kong alikokuwa akitumikia kifungo cha miaka 10.
“Ametoka jela miezi mitatu iliyopita, lakini amekamatwa tena na heroin akiwa Bandari ya Dar es Salaam,” alisema.
Aliongeza; “Mtuhumiwa anasema alitumwa na mtu anayeitwa Salehe Ally Issa, mkazi wa Mbezi.”
Kamishna Milanzi alisema baada ya kumkagua walimkuta na hati mpya ya kusafiria ya kielektroniki ambayo mtuhumiwa alidai ametengenezewa na Issa ili imsaidie kusafirisha dawa nchi mbalimbali.
Milanzi alisema Issa pia alikamatwa Mei 24 mwaka huu nyumbani kwake.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment