Imeelezwa kuwa Kiwango cha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi Kitaifa yameshuka kutoka asilimia 7 mwaka 2013/2014 hadi kufikia asilimia 4.7 mwaka 2016-2017.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango mkakati wa nne wa Virusi vya UKIMWI na UKIMWI katika Sekta ya Afya (HSHSP IV 2017-2022) Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema Wizara kwakushirikiana na wadau mbalimbali Kitaifa na Kimataifa itaendelea kuchukua juhudi za makusudi ili kuhakikisha adui UKIMWI unatokomezwa hapa nchi.
Waziri Ummy aliongeza kuwa Desemba 2017 Tanzania ilizindua ripoti ya awali ya utafiti wa Kitaifa wa matokeo ya UKIMWI wa mwaka 2016/2017 ulioonesha kiwango cha maambukizi ya VVU kimeshuka kutoka asilimia 5.1 mwa 2011/12 hadi kufikia asilimia 4.7 mwaka 2016/17 hivyo kufanya kiwango cha maambukizi Kitaifa kushuka kwa asilimia 0.4 tu kwa takribani miaka mitano.
Waziri Ummy Amesema kuwa kupungua kwa asilimia 0.4 tu kunawezekana kuwa na taswira mbili, kuwa kiwango hiki cha kupungua maambukizi ya VVU kitaifa ni kidogo kwa miaka mitano na hivyo si jambo la kujivunia kama taifa, ama kwa upande mwingine inawezekana kuwa dawa za kupunguza makali ya VVU zinatumika vizuri na hivyo kuleta mafanikio yaliyotegemewa ya kupunguza vifo vitokanavyo na VVU na UKIMWI na hivyo WAVIU kuishi maisha marefu ya kawaida.
Aidha, Waziri Ummy alisema kuwa Ripoti ya Utafiti wa Kitaifa wa Matokeo ya UKIMWI wa mwaka 2016 – 2017 inaonesha kwamba, asilimia 12 ya vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 nchini wanaanza ngono kabla ya kufikisha umri wa miaka 15; ambapo kwa wanaume ni asilimia 14 na wanawake ni asilimia 9.
Ili kukabiliana na hatari ya VVU na UKIMWI kwa Vijana Waziri Ummy amesema kuwa Mpango Mkakati aliouzindua pamoja na mambo mengine, unaweka msisitizo katika kutekeleza, afua zinazowalenga vijana hasa wa kike ambao wapo katika hatari zaidi ya kuambukizwa VVU kutokana na sababu za kibaiolojia, kiuchumi na kimila.
Waziri Ummy alisema kuwa Wizara yake imetoa mwongozo mpya na wameanza utaratibu wa kuanzisha dawa za ARV kwa WAVIU ndani ya wiki mbili ili kuongeza kasi idadi ya watu wanaotumia dawa za ARV na hivyo kuwafanya wawe na afya ya kuwawezesha kuendelea na shughuli zao za kila siku.
Pia, Waziri Ummy aliwataka Waganga Wakuu wa Mikoa na baadhi ya Waganga Wakuu wa wilaya kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za upimaji VVU katika mikoa na wilaya zao sambamba na kutumia mbinu na njia mbalimbali kuwapatia huduma za upimaji VVU, watu wanaoishi na VVU ambao hawatambui hali zao za maambukizi.
Waziri Ummy alitoa rai kwa watanzania kujitokeza kupata huduma ya Upimaji VVU, huduma inayopatikana bila malipo nchi nzima, mijini na vijijini na iwapo utagundulika kuwa una VVU, utaanzishiwa dawa za ARV mapema ikiwa dawa za ARV zinapatikana na zinatolewa bure katika vituo vya huduma za tiba na matunzo vipatavyo 6,259 nchi nzima
chanzo:BONGO5
chanzo:BONGO5
No comments:
Post a Comment