Atafutwa na Jeshi la Polisi kwa kumchinja mke na mtoto wake wa mwaka mmoja
Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Omari Matonya anatafutwa na jeshi la Polisi mkoani Tabora kwa tuhuma za kuwaua kwa kuwachinja mke wake na mtoto wao, kisha kukimbia.
Akizungumza leo kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora Wilbroad Mutafungwa amesema kwamba mtu huyo amefanya tukio hilo nyakati za usiku wakati wakiwa wamelala, huku chanzo kikubwa kikitajwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.
“Mwanamke ambaye anaitwa Moshi Daudi mwenye miaka 24 akiwa na mtoto wake wa mwaka mmoja anayeitwa Omari Matonya, waliuawa kwa kuchinjwa na kitu chenye ncha kali shingoni na mwanaume anaitwa Omari Matonya mwenye miaka 25, ambaye ni mume wa huyo mama na baba mzazi wa huyo mtoto, baada ya kufanya tukio hilo alitoweka.
Alifanya tukio hilo wakati familia yake ikiwa imelala na chanzo kikitajwa kuwa ni wivu wa mapenzi, ambapo huyo marehemu alikuwa akituhumiwa kuwa na mahusiano na shemeji yake, ambaye ni ndugu yake huyo Matonya anayeitwa Lazima Matonya”, amesema Kamanda Mutafungwa.
Kamanda Mutafungwa amesema mpaka sasa hajapata taarfa zake zozote na jeshi la polisi linaendelea kumtafuta, ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
No comments:
Post a Comment