Dodoma. Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amesema kampuni ya madini ya Tanzanite One imeshailipa Serikali malipo ya awali ambayo hayatawekwa wazi.
Amesema mbali na malipo hayo, mazungumzo kati ya kampuni ya kuchimba madini ya Barrick na Serikali yanaendelea vizuri na katikati ya Juni na Julai, 2018 watakuwa wamfikia hatua za mwisho.
Profesa Kabudi ameeleza hayo leo Ijumaa Juni 1, 2018 katika mjadala wa bajeti ya Madini ya mwaka wa fedha wa 2018/19.
Amesema mazungumzo kati ya Serikali na Tanzania One yalikamilika Aprili 15, 2018.
“Wamekili na kulipa kodi na tozo zote na watatoa fidia na tayari malipo ya kwanza wamelipa. Tunaishi kwa kujifunza, tukitaja watajua wanaotudai watafungua kesi zingine,” amesema.
“Lakini ndani ya Serikali Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) atajua na zinasimamiwa na Katiba Mkuu Kiongozi na tumejifunza hatutatamka katika kadamnasi, ni upuuzi kusema na tukisema watafungua kesi nyingine.”
Kuhusu Barrick amesema mazungumzo hayo yaliyoanza Oktoba 19, 2017 yamekuwa na tija kwa madini hayo kunufaisha nchi kwa kizazi cha sasa na kijacho.
“Kuangalia Tanzania ya kesho ya madini, tumerithi mikataba iliyokuwa na matatizo makubaliano yalikuwa ya msingi na yanaendelea vizuri kati ya Serikali na Barrick na mwisho wa Juni au Julai tutakuwa tumefikia hatua za mwisho,” amesema.
Amesema lengo ni Serikali kuzungumza na kampuni mbalimbali za uchimbaji madini ili nchi kunufaika na rasilimali hizo, kwamba utaratibu wa sasa leseni zitatolewa kwa masharti ya baraza la mawaziri na kusisitiza kuwa asiyetaka asije nchini kuwekeza.
No comments:
Post a Comment