KESHOKUTWA Jumapili shughuli nyingi sana zitasimama, kama itakuwa ni rasmi au kimyakimya lakini kwa kuwa watani wa jadi Simba na Yanga wanakutana, kwa anayependa mpira, lazima atakuwa anataka kufuatilia kwa ukaribu.
Simba na Yanga maarufu kama Kulwa na Dotto watakuwa wanakutana katika mechi ambayo itaamua mambo mengi ya Ligi Kuu Bara ambayo kama mmoja atapoteza, atakuwa amekuwa ametengeneza jambo ambalo litakuwa linatengeneza ugumu kwake.
Kama Simba itashinda, maana yake itakuwa imefikisha pointi 62 na kuifanya Yanga izidi kukata tamaa kupambana na kuipata, hivyo itakuwa imejiwekea mazingira mazuri ya kutangaza ubingwa kama itaendelea kucheza karata zake vizuri katika mechi nyingine mbili tu za mbele.
Yanga nayo ikishinda, itakuwa imetengeneza mambo mawili muhimu kwao, kwanza ikiwa ni kujiweka katika nafasi nzuri ya kuikamata Simba na pili, kuamsha presha upande wa pili ambayo kama wakishindwa kuidhibiti, basi wapoteze mwelekeo.
Hizo zikawa hesabu za kila upande kwa timu kwa maana watakuwa wanataka kushinda kwa gharama yoyote ile. Hivyo lazima wako makini sana katika maandalizi yao kabla ya mchezo huo wa keshokutwa.
Wakati hao wanafanya hivyo, suala linafuatia kwa wale ambao watakuwa wanakwenda uwanjani kwa ajili ya kushuhudia burudani hiyo ya watani wa jadi.
Mechi ambayo itakuwa na uamuzi wa mambo mengi sana kuhakikisha yanakwenda kuonekana hadharani. Mashabiki watakaokwenda uwanjani ndio ninaotaka kuzungumza nao leo kwamba wanakwenda kwa ajili ya burudani.
Wao wanachokifuata ni kuburudika pia kuziunga mkono timu zao ili kuhakikisha zinaibuka na ushindi kwa kuwa kila mmoja anajua faida za ushindi ni ipi baada ya mchezo huo kama nilivyokutajia hapo mwanzo.
Kazi ya kushangilia si lazima kutukanana, wala kazi ya kushangilia si lazima kuumizana. Mashabiki wengi wa mpira hapa nyumbani, wamekuwa na tabia ambazo si za kiungwana ambazo husababisha wengine kuumia au kupata matatizo.
Shabiki anayeamini kumtukana mwenzake ndiyo ushabiki, au kumpiga na kumuumiza mwingine ndiyo furaha, ni ujinga wa kupindukia ambao tumekuwa tunaendekeza na unapoteza maana ya upenzi wa mpira.
Kumbuka kila aliye uwanjani hapo ni mwanadamu muhimu kama si kwako basi kwa ndugu zake.
Kumbuka kila aliyekuja uwanjani ana haki ya kufurahia na kurejea nyumbani akiwa salama. Hivyo, kila mmoja anapaswa kuheshimu utu wa mwenzake.
Ushabiki mnaweza kuzodoana, kutaniana na baada ya mechi mkakumbatiana, kumpoza aliye na majonzi ya kupoteza, kumpongeza aliyeibuka na ushindi au kupeana pole na hongera baada ya sare.
Nimeeleza mara nyingi sana kuhusiana na mashabiki kuonyesha wao wanazipenda timu nyingine huku wakitaka na wengine waone kwamba wanazipenda kweli.
Ushabiki unakuwa si kwa sababu ya mhusika, badala yake hata furaha yake, anataka ionekane kwa wengine ndiyo ikamilike.
Hivyo, kama ni shabiki wa Simba, akimtukana wa Yanga mbele ya mashabiki wengine wa Simba anaona kama amefanya jambo kubwa sana la kusifiwa, hali kadhalika wa Yanga akifanya hivyo kwa yule wa Simba.
Unaona Afrika Kusini, mashabiki wa Kaizer Chiefs na Orlando Pirates wanachanganyika siku ya mechi, tunaona Rwanda, Rayon Sports na APR wanakuwa pamoja na hakuna kutukanana badala yake ni ubishi wa mpira.
Sisi hatufanyi hivyo, haina maana ni utamaduni kupigana. Badala yake hatukuwa sahihi na tunapaswa kubadilika.
Kwenda uwanjani na kurudi salama ni jambo jema, kushinda au kupoteza na hata ikiwa sare ni mambo ya mpira. Itakuwa vizuri kama mtaonyesha nyie ni mashabiki wa timu kongwe na mna mawazo chanya kuhusiana na mpira na upendo badala ya mpira kuwa uadui tu.
No comments:
Post a Comment