Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa amekutana na maafisa wa usalama Jumapili wakati uchunguzi unaendelea kufanywa na vyombo vya dola kutafuta kiini cha shambulizi hili na vishawishi vilivyopelekea mtu huyu (miaka kati ya 20-21) kuwashambulia watu katika mitaa ya mjini Paris Jumamosi usiku, na kumuuwa moja wao.
Kikundi cha Islamic State kimedai kuhusika na tukio hili katika mji mkuu wa Ufaransa.
Maafisa wa serikali ya Ufaransa wamepongeza hatua za haraka zilizochukuliwa na polisi hapa, ambao walifika katika eneo la tukio hilo dakika chache tu baada ya kutokea shambulizi hilo kufuatia kelele ya kwanza kabisa ya kuomba msaada.
Polis wanasema kuwa bila ya kupoteza muda maafisa wa polisi walimpiga risasi na kumuua mshukiwa huyo aliyekuwa akishambulia watu, ambapo hapo awali walipofika tu walijaribu kumdhibiti kwa kutumia kifaa kingine.
Mwendesha mashtaka wa Paris Francois Molins amewaambia waandishi wa habari kuwa mshukiwa huyo alitamka “Allahu Akbar” wakati akiwashambulia watu na kisu. Amesema wachunguzi wanafuatilia tukio hilo kwa kushukiwa kuwa kulikuwa na hamasisho la kigaidi.
Maafisa wanasema kuwa mshukiwa huyo alimuuwa mtu moja na kuwajeruhi wengine wanne. Wazazi wake wanashikiliwa na polisi kwa ajili ya kuhojiwa. Taarifa zaidi zinasema mshukiwa huyo alizaliwa nchini Chechnya mwaka 1997 na baadae kupata uraia wa Ufaransa.
No comments:
Post a Comment