Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, imewafukuza zaidi ya mahakimu 250 ambao waliajiriwa kwa kutumia vyeti feki na wengine waliotuhumiwa kupokea hongo.
Kumeundwa tume maalum itakayo fuatilia idara mbalimbali kwa kuchunguza maafisa ambao hawatimizi vigezo na masharti ya kufanya kazi kama mahakimu au wizara nyingine.
Mahakimu hao wamefukuzwa na raisi Kabila, kwa kile alicho kisema ni kosa la kutumia vyeti bandia na wengine kwa tuhuma za kupokea rushwa wakati wa kesi mbalimbali.
Hatua hii inafuata malalamiko mengi kutoka kwa raia na pia kwa kutathmini utendaji kazi wao usio na ubunifu.
Mara kwa mara mashirika ya kiraia yamekuwa yakilalamika kuhusu utendaji kazi wa mahakama nchini na hatua ya kuwatimua inaonekana kuwa moja ya majibu anasema Dufina Tabu mratibu wa shirika la kutetea hai za binaadamu nchini Congo - Savoco.
'Tulikuwa tukimuandikia rais barua zetu, na inaonekana zimefika. Kwa hivyo inakuwa ni mfano mzuri.
'Maskini kupata haki yake kisheria ni vigumu sana. Kila kitu ni pesa. Watu wanateswa sana katika kupata haki, na tutaendelea kumuunga mkono rais. Kwa yoyote atakayefanya makosa tutamuandikia, tumtaje na aadhibiwe kabisa ili tuweze kuisaidia nchi yetu kupona'.
Hata hivyo, waziri wa sheria Alexi Tambwe Mwamba amesema kwamba kumekuwa na tume maalum ilioundwa kuendesha uchunguzi zaidi ilikuwagundua mahakimu wengine feki.
Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo, inayo jumla ya mahakimu 4000 upande wa kiraia pamoja na kijeshi walioajiriwa kwa misingi ya mashindano ya kitaifa.
Lakini inaonekana mchakato huo ulikumbwa na kasoro za rushwa kwa mujibu wa tangazo la serikali.
Mara kwa mara rais Kabila ametangaza uwajibikaji wake katika kukabiliana na rushwa nchini Congo, lakini wakosoaji wamekuwa wakiona kwamba hakuna ishara wala azma ya kisiasa na pia uthibitisho wa hatua kupigwa katika kukabilaina na hilo kando na kuundwa sheria kali, ambazo mara nyingi hazifuatwi.
Shirika la kimataifa la kutetea haki za kibinaadamu Transparency International linasema ajenda ya kupambana na rushwa mara nyingi huingiliwa kati kwa maslahi ya kisiasa.
Changamoto katika idara ya mahakama:
Idara ya mahakama nchini DRC inakabiliwa na changamoto nyingi.
Rasilmali ni finyu kwa mahakama za nchi hiyo ambayo imeshuhudia vita vya kiraia kwa muda sasa. Idadi ya maafisa wa kutosha na uhuru wake - hatua inayoonekana kuathiri uwezo wake kuchukua hatua dhidi ya rushwa.
Na hiyo inamaanisha kuwepo kwa maafisa wasiotosha kukabiliana na mzigo wa sheria nchini na pengine ndio kukawepo mwanya wa kuishia kuajiriwa majaji hao 'feki' kama hawa wa sasa 250 waliotimuliwa na rais Kabila.
Katiba ya nchi hiyo inatoa muelekeo wa wazi wa uongozi tofuati nchini.
Kisheria, Rais ndiye anayewaandika na kuwafuta maafisa katika idara hiyo ya mahakama.
Hii sio mara ya kwanza kwa kiongozi huyo mkuu kuchukua hatua dhidi ya maafisa wa idara ya mahakama nchini - mfano mnamo 2008 rais Kabila aliwalazimisha majaji 89 kustaafu akiwemo kiongozi mkuu wa mahakama ya juu zaidi , na mwendesha mkuu wa mashtaka na badala yake akawaajiri majaji wengine 28 kuzichukua nafasi hizo.
Hatua hii wakati huo alidai pia ni katika kukabiliana na jinamizi la rushwa nchini lakini haikupokewa vizuri na baadhi ya wachambuzi walioona ni kama hatua isiyostahili maana inaingilia kati mfumo wa idara ya mahakama.
No comments:
Post a Comment