KOCHA Mkuu wa Yanga, Mkongoman Zahera Mwinyi ni kama ameshaanza kazi kikosini hapo.
Tayari yupo Morogoro akiwa na kikosi hicho mazoezini ambapo taarifa zinaeleza kuwa amevutiwa na viwango vya wachezaji aliowakuta.
Nikukumbushe siku kadhaa zilizopita wapenzi na mashabiki wa Yanga walipigwa na butwaa baada ya aliyekuwa kocha wa timu yao, Mzambia, George Lwandamina kuondoka ‘kimyakimya.
Ndani ya Yanga, Lwandamina alipokea kijiti kutoka kwa Mholanzi, Hans van Der Pluijm ambaye kwa sasa anakinoa kikosi cha Singida United kinachoshiriki Ligi Kuu Bara.
Kocha huyo msimu uliopita alifanikiwa kuipa Yanga ubingwa ukiwa ni msimu wake wa kwanza ndani ya kikosi hicho, ingawa msimu huu kidogo mpaka ligi ilipofika mambo yameonekana kuyumba ingawa ligi bado haijamalizika.
Lwandamina alipambana na kuweza kuibeba Yanga tangu alipoanza kuinoa msimu uliopita ambapo alitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na timu yake ikafanikiwa kushiriki michuano ya kimataifa ambayo mpaka sasa inashiriki na Jumatano ijayo timu hiyo itacheza bila yeye dhidi ya Wolaitta Dicha.
Katika mchezo wa kwanza hapa nyumbani dhidi ya Wolaitta Dicha ya Ethiopia kwenye Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya mtoano, Lwandamina alikuwepo kwenye benchi wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Pamoja na kuondoka kwake Yanga alikuwa ni moja kati ya makocha ambao walichangia kukuza vipaji vya wachezaji wengi na kuweza kufika hapo walipo sasa.
Pia ni mmoja kati ya makocha wa kigeni ambao wanastahili kupongezwa kutokana na aina ya ufundishaji wake pamoja na falsafa yake ya kuweza kuwaamini vijana.
Mzambia huyo alifanikiwa kuwatumia vijana katika kikosi chake ambao awali hawakuwa wakipewa nafasi ndani ya kikosi hicho na wengine aliweza kuwasajili baada ya kubaini uwezo wao. Mfano Yohana Nkomola na Ramadhani Kabwili ambao walitoka Serengeti Boys.
Kocha huyo alikuwa akiwapa nafasi vijana hao pamoja na wengine kikosini hapo na walipambana kweli na hawakuweza kumuangusha.
Kwa msimu huu, vijana wengi ndani ya kikosi cha Yanga wamepewa nafasi kubwa baada ya wazoefu kuwa nje wakiuguza majeraha.
Baada ya kocha kuondoka bado Yanga ina kibarua kizito kuhakikisha inajipanga sawa kwa kupata matokeo kwa michezo ambayo iko mbele yao bila hivyo itakuwa ngumu kwao kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Bara.
Licha ya kuondoka kwa kocha huyo ndani ya Yanga, viongozi wa timu hiyo wanapaswa kujipanga na kujijenga kisaikolojia kwa kuhakikisha timu yao inafanya kweli kwenye michuano iliyopo mbele yao hasa upande wa kimataifa ambapo wameshafuzu kucheza Hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Tunafahamu Yanga inapitia kipindi kigumu kutokana na kuwa na lundo la majeruhi ambao wapo nje kwa muda mrefu wakijiuguza na kulazimika kuwatumia vijana ambao hawana uzoefu kwenye michuano ya kimataifa.
Sasa pamoja na hilo inatakiwa kujiamini kuwa inaweza kufanya vyema kwa kupitia haohao vijana ili iwe mfano kwa timu zingine kutoogopa kuwatumia.
Hivyo kocha mpya huyo Mcongo anaweza kuwa na falsafa yake pengine ya kuendelea kuwatumia au kuwaweka kando ili wajifunze zaidi lakini tumeona umuhimu wao kikosini.
No comments:
Post a Comment