Kwa ufupi
- Watumishi wa umma ambao awali walikuwa wanafanya marejesho mpaka miaka sita ambayo ni sawa na miezi 72, sasa wanaruhusiwa kufanya hivyo mpaka miezi 84.
Dar es Salaam. Benki ya CRDB imeongeza muda wa marejesho kutoka miezi 60 hadi 84 huku ikishusha riba kwa asilimia nne kwa wateja wake, hasa wafanyakazi.
Benki hiyo imeshusha riba kutoka asilimia 21 mpaka 17 huku muda wa marejesho ukitofautiana kati ya wafanyakazi wa sekta binafsi na watumishi wa umma.
Wateja wa benki hiyo wameanza kunufaika na punguzo hilo tangu wiki iliyopita pindi menejimenti iliporidhia kufanya mabadiliko hayo.
Akizungumza na Mcl Digital leo Mei 13, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Dk Charles Kimei amesema mabadiliko hayo yanalenga kumpa mteja unafuu wa kukamilisha malengo yake kwa wakati.
“Punguzo hili linatolewa kwenye matawi yetu yote. Tangu wiki iliyopita huduma hiyo imeanza kupatikana,” amesema Dk Kimei.
Watumishi wa umma ambao awali walikuwa wanafanya marejesho mpaka miaka sita ambayo ni sawa na miezi 72, sasa wanaruhusiwa kufanya hivyo mpaka miezi 84 au miaka saba wakati wafanyakazi wa sekta binafsi waliokuwa na miaka mitano wameongezewa mpaka miaka sita.
Hatua ya CRDB imekuja baada ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kushusha riba ya mikopo inayotoa kwa benki za biashara mara mbili mfululizo.
Machi mwaka jana, ilipunguza riba hiyo kwa asilimia nne kutoka asilimia 16 mpaka 12.
Mwaka mmoja baadaye, BOT ilipunguza tena kwa asilimia moja na kushusha kiwango cha akiba ambacho benki hizo zinatunza kwake kutoka asilimia 10 mpaka nane ili kuzipa uwezo zaidi wa kuikopesha sekta binafsi.
No comments:
Post a Comment