Jeshi la Polisi limeanza kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya watu wanaoichafua serikali kwa kusambaza vitabu vya wanafunzi wa shule ya msingi visivyo sahihi mitandaoni.
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Simon Sirro amesema Ijumaa mjini Dodoma, Tanzania kuwa amepokea maagizo ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako na wameanza kuchukua hatua.
“Agizo tumelipokea vizuri baada ya taarifa kuja kwetu, tutafungua jalada tutapeleleza na kubaini aliyetuma vitabu hivyo kwenye mtandao,” alisema Sirro.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari nchini humo wakati akijibu mwongozo wa Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Martha Mlata, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Ndalichako alisema kitabu cha Kiingereza kilichosambaa ni cha darasa la tatu kilichokuwa na makosa na kimekwisha ondolewa na waliosababisha wamechukuliwa hatua.
Alisema kitabu cha Kiswahili kinachoonyesha mwili wa binadamu, hakijawahi kuwa sehemu ya vitabu vya kiada na hajui ni kina nani wanavisambaza na kwa malengo gani.
“Kwa kuwa vyombo vya ulinzi na usalama viko hapa, naviagiza mara moja vitafute mara moja watu wanaotengeneza na kuichafua serikali na hatua zichukuliwe,” alinukuliwa Profesa Ndalichako.
Akizungumza Mei 4, mwaka huu, wakati akijibu mwongozo wa Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Martha Mlata, aliyetaka kujua hatua ambazo serikali inazichukua kwa kuwa kumekuwa na vitabu vya ovyo vinasambaa mitandaoni.
No comments:
Post a Comment